Kupitia Ibada Maalum ya Kumwombea aliyekuwa Waziri Mkuu Mh. Hayati Edward Lowassa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Alex Malasusa, Azungumzia Utamaduni wa Kuaga Mwili.
Katika ibada maalum ya kumuombea marehemu Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, iliyofanyika leo Februari 14, 2024, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, ametoa msimamo kuhusu utamaduni wa kuaga mwili. Malasusa amesisitiza kwamba hakuna ulazima kwa kanisa kufungua jeneza ili waumini waone mwili wa mwanadamu aliyefariki, akibainisha kuwa hiyo siyo sheria wala taratibu za kanisa.
“Tuwe tunatazamana tukiwa hai tusisubiri mtu amelala. Msifikiri kwenda kuaga lazima ufungue jeneza mtu wamuone; siyo lazima,” alisema Malasusa.
Kauli hii imetolewa leo tarehe 14/2/ katika ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Edward Lowassa, aliyefariki dunia Februari 10, 2024, kauli ikilenga kuhamasisha umuhimu wa kuthaminiana na kushirikiana katika uhai badala ya kusubiri hadi mtu amefariki. Malasusa ametumia fursa hii kutoa wito kwa waumini na jamii kwa ujumla, kudumisha upendo na mshikamano wakati wote.