Atumia Saa 1:30 Kupanda Jengo La Ghorofa 101
Mpanda majengo marefu na miamba hatari maarufu
wa Marekani, Alex Honnold, amefanikiwa kupanda jengo refu la
ghorofa 101 jijini Taipei, Taiwan, bila kutumia kamba, mkanda wa
usalama wala vifaa vyovyote vya kujilinda.
Jengo hilo lijulikanalo kama Taipei 101 lina urefu wa mita 508 na
limejengwa kwa chuma, kioo na zege, likiwa na muundo
unaofanana na shina la mianzi, jengo hili ndilo lililoshikilia kuwa
jengo refu zaidi duniani kwa mwaka 2004 hadi 2009 ambapo
sasa linashikilia nafasi ya 11 duniani na ndilo jengo refu zaidi
Taiwan likishika nafasi ya kwanza.
Honnold, anayejulikana duniani kwa kupanda miamba kwa
mtindo hatari wa free solo, aliweka historia hapo awali kwa
kuwa mtu wa kwanza kupanda jabali la El Capitan lenye urefu
wa mita 915 katika Hifadhi ya Taifa ya Yosemite, California, bila
kamba wala vifaa vya usalama na kupelekea kushinda tuzo ya
Oscar.
Safari yake ya kupanda Taipei 101 ilikuwa imepangwa kufanyika
Jumamosi, lakini ilicheleweshwa kutokana na mvua.
Upandaji huo ulirushwa mubashara na Netflix, ambayo ilisema
kulikuwa na ucheleweshaji mdogo wa matangazo ili kuzuia
kuonyesha tukio lolote baya endapo lingetokea "Tungekatisha
matangazo," alisema mmoja wa wakuu wa Netflix, Jeff Gaspin,
akinukuliwa na jarida la Variety kabla ya tukio hilo na kuongeza
kuwa "Hakuna anayetarajia wala kutamani kuona jambo baya
likitokea."
Honnold alikamilisha upandaji huo kwa muda wa saa moja na
dakika 31 siku ya Jumapili Januari 25, akivunja rekodi ya awali
kwa zaidi ya nusu ya Mfaransa Alain Robert, anayejitambulisha
kama "Spiderman", ndiye aliyewahi kupanda jengo hilo hapo
awali kwa saa nne, akitumia kamba na mkanda wa usalama.
Makamu wa Rais wa Taiwan, Hsiao Bi-khim, alimpongeza
Honnold kupitia mtandao wa X akisema, "Nakiri, ningejisikia
kichefuchefu pia, hata kuangalia ilikuwa vigumu" Honnold
alikaribishwa juu ya jengo hilo na mke wake, ambaye alieleza
kuhusu upepo na joto wakati wa upandaji.

No comments