Wema Sepetu na Whozu Wapata Mtoto
Mwigizaji nguli wa filamu na Mwanamitindo, Wema Sepetu na mchumba wake Oscar Lelo ‘Whozu’ wameweka wazi kuwa wamepata Mtoto wa Kiume, habari iliyopokelewa kwa furaha kubwa na Mashabiki wao pamoja na Wadau wa burudani.
Wema na Whozu, ambao wamekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa takribani miaka minne, walithibitisha ujio wa Mtoto wao leo Juni 13, 2026 kupitia kurasa zao za Mitandao ya Kijamii kwa kushiriki ujumbe wenye hisia na shukrani kwa Mungu.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Wema alichapisha picha ya mguu wa Mtoto huyo huku akiandika maneno yanayoashiria furaha na mshangao wa kuona ndoto yake ya kuwa Mama ikitimia.
Naye Whozu aliandika;
“Sio kuwa tu wazuri sana mbele zake lakini ilimpendeza aonyeshe ukuu wake kwenye uso wa dunia kuwa makadirio ya Wanadamu hayawezi kushinda kudra zake… Hakika Mwenyezi Mungu amejidhihirisha na kutupa kibali, Hongeraa Shunu wangu na Akhsanteni nyote mliokuwa mkituombea, Mungu Yupo na wanaomtumaini tusichoke kukesha tukiomba maana yeye ni mwenye huruma siku zote 12/6 #PUBLIC HOLIDAY.”
Kwa upande wa Whozu, huyu anakuwa Mtoto wake wa pili baada ya yule wa kwanza aliyempata na Tunda, huku kwa Wema Sepetu akiwa Mtoto wake wa kwanza, jambo ambalo limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wake wengi.
